Total Pageviews


Breaking News

Friday, January 30, 2015

Sasa Yanga ni full raha





MASHABIKI wa Yanga  jana Jumatano walikuwa na furaha kuliko wale wa Mbeya City ambao timu yao iliifunga Simba mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ipo hivi; mashabiki wa Yanga wanaamini kufanya vibaya kwa Simba ni neema katika harakati zao za kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Kwa ushindi ilioupata, Mbeya City imepanda mpaka nafasi ya saba kutoka ya 12 ikiwa na pointi 15 huku Simba ikishuka hadi nafasi ya 11 kutoka ya kumi, imebaki na  pointi 13 zake.
Mchezo wa jana ulijaa upinzani mkali kutokana na rekodi za timu hizo msimu uliopita ambapo katika mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 pamoja na 2-2.
Hadi ilipoingia  dakika ya 90 jana, timu hizo zilikuwa sare kwa bao 1-1 na tayari baadhi ya mashabiki walishaanza kutoka uwanjani wakiamini mchezo ungemalizika kwa sare hiyo, kabla ya mambo kubadilika kwenye dakika za majeruhi ambapo Watoto wa Mbeya wakashinda kwa bao la penalti.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alisema: “Mwanzo wachezaji wangu hawakuwa makini, lakini tulipoenda mapumziko niliwataka watulie na kuwaeleza tatizo la Simba,  nashukuru walifanya nilivyotaka. Lakini mwamuzi aliipa Simba penalti isiyo halali lakini pia nashukuru wakakosa, sasa tunatazama mechi zijazo.”
Naye Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema: “Kilichotuponza katika mechi hii ni kuridhika na bao moja la kuongoza ndiyo maana nikawatoa akina Sserunkuma (Dan na Simon), lakini bado hawakuweza kupambana kuongeza bao lingine.”
Awali Simba ilianza mchezo  kwa kasi na kutawala sehemu ya kiungo ambapo Jonas Mkude alimzidi uwezo kiungo mkongwe wa Mbeya City, Steven Mazanda. Uwezo huo wa Simba uliiwezesha kupata bao dakika ya 23 lililofungwa na Ibrahim Ajib kwa faulo iliyopigwa nje kidogo ya eneo la hatari. Faulo hiyo ilitolewa na mwamuzi Abdallah Kambuzi wa Shinyanga baada ya Awadh Juma kuchezewa vibaya na Hamad Kibopile.
Katika dakika za 25 na 35 timu zote zilipoteza nafasi, ilianza Simba pale Ramadhan Singano alipopiga nje kabla ya Paul Nonga kupanguliwa kiki yake na kipa wa Simba, Manyika Peter.
Kipindi cha pili Simba  iliwatoa Dan Sserunkuma, Ajib na Simon Sserunkuma na nafasi zao kuchukuliwa na Elius Maguli, Abdi Banda na Ibrahim Twaha.

No comments:

Post a Comment

Designed By MR.PRIME 2015