Total Pageviews


Breaking News

Saturday, January 31, 2015

Simba wamuwashia moto Juma Nyosso


Beki wa Mbeya City Juma Nyosso.

SIKU moja baada ya Gazeti la Championi kutoa picha ya beki wa Mbeya City, Juma Nyosso akionekana kumfanyia ndivyo sivyo straika wa Simba, Elias Maguri, makubwa yameibuka.

Uongozi wa Simba na Maguri wote kwa pamoja wametoa kauli juu ya tukio hilo na kulikemea kwa nguvu huku wakilishukuru gazeti hili kwa kutoa picha hizo kwa kuwa Watanzania na jamii nzima imejua ‘uchafu’ ambao unafanyika kwenye Ligi Kuu Bara.
Evans Aveva ambaye ni rais wa Simba, amesema tukio hilo lililotokea wakati wa mechi baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, ni la kidhalilishaji na kudai matukio kama hayo yanapingwa kwa nguvu zote na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
“Sijui sana kuhusu maadili ya uandishi wa habari lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya wachezaji kama hao.“Kimsingi suala hili la kuchapishwa picha za tukio alilofanyiwa Maguri katika Gazeti la Championi siwezi kulizungumzia kitaaluma.
“Lakini tunakikemea vikali kitendo hicho, kwani tumesikitishwa sana. Hii ni changamoto kwa TFF na klabu kuhakikisha tunakwenda sambamba na teknolojia, tusisubiri mpaka ripoti za waamuzi ndipo tufanye maamuzi.
“Mfano ni suala la Suarez alipomng’ata mchezaji wa Italia, Fifa ilimfungia baada ya kutumia teknolojia na haikutumia ripoti ya waamuzi pekee. Matukio mabaya yamejitokeza kwa (Amissi) Tambwe, (Emmanuel) Okwi na Maguri, pia huko daraja la kwanza ndiyo usiseme.
“Ninavishukuru vyombo vya habari kwa kuweza kuibua mambo hayo ili yaweze kuchukuliwa hatua na kukomeshwa kabisa,” alisema Aveva.  Akizungumzia tukio hilo, Maguri alikuwa na haya ya kusema: “Kwanza nikwambie tu ile ishu imenidhalilisha sana kwa watu wengi maana imekuwa ‘topic’ kubwa katika mitandao ya kijamii. Kwa hiyo mimi binafsi na familia tunalichukulia kama tukio baya sana kwangu kwani limetudhalilisha.
“Siwezi kuliacha hivihivi, lazima nilichukulie hatua lakini kwa vile TFF na wahusika wengine wameliona, ninasubiri kwanza kuona hatua gani watachukua, kama sitaridhika nazo ndipo nitakapojua nini cha kufanya.“Nashukuru mpigapicha wenu kwa kuwa alifuatilia na kuliona tukio vizuri japokuwa ni la aibu.” 

No comments:

Post a Comment

Designed By MR.PRIME 2015